KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Wednesday, August 17, 2011

Diego Forlan KUFUNGULIWA MILANGO ATLETICO MADRID?

Klabu bingwa duniani Inter Milan imeonyesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Uruguay pamoja na klabu ya Atletico Madrid ya nchini Hispania Diego Forlan.

Inter Milan wameonyesha nia hiyo kufuatia mipango yao ya kumuuza mshambuliaji kutoka nchini Cameroon Samuel Eto’o kukaa vizuri na wanaamini Diego Forlan, atakua jibu sahihi la kuziba nafasi yake.

Hata hivyo tayari uongozi wa Atletico Madrid umeshaeleza wazi kwamba kuuzwa kwa mshambuliaji huyo aliekiongoza kikosi cha timu ya taifa ya Uruguay kutwaa ubingwa wa fainali za mataifa ya Amerika ya kusini COPA AMERICA mwaka huu, kutategemea na kukamilishwa kwa mipango ya kusajiliwa kwa mshambuliaji kutoka nchini Colombia pamoja na Fc Porto Radamel Falcao.

Katika hatua nyingine uongozi wa Atletico Madrid umedai kwamba mbali na Inter Milan kutuma ofa ya kutaka kumsajili Diego Forlan, pia wamepokea ofa nyingine kutoka kwenye klabu ya Galatasaray ambayo ilionyesha lengo hilo toka mwezi uliopita.

Siku za hivi karibuni Diego Forlan, alikaririwa na vyombo vya habari ambapo alionyesha mapenzi ya kutaka kuishi nchini Uturuki huku akidai kwamba nchi hiyo ina mazingira mazuri na yenye kupendeza, hivyo angependa siku moja aishi huko.

Kauli hiyo imezusha hofu kwa mashabiki pamoja na viongozi wa Inter Milan kwa kudhani huenda wakamkosa lakini bado inaaminiwa lolote laweza kutokea na akakubali kuelekea Stadio Guissepe Meaza kabla ya August 31.

Inter Milan kwa sasa wanamsaka mrithi wa Samuel Eto'o ambae yu njiani kujiunga na klabu ya Anzhi Makhachkala iliyopania kufanya mapinduzi ya soka ya nchini Urusi.

Wakati huo huo raisi wa Inter Milan Massimo Moratti amemaliza zogo la kiungo kutoka nchini Uholanzi na klabu hiyo Wesley Sneijder anaehusishwa na taarifa za kutaka kusajiliwa na moja ya klabu za mjini Manchester nchini Uingereza kwa kusema mchezaji huyo hatouzwa.

Massimo Moratti amemaliza zogo hilo kwa kutoa kauli iliyo thabit alipokutana na vyombo vya habari kwa ajili ya kumtakia kila la kheri mshambuliaji Samuel Eto’o ambae anajiandaa kujiunga na klabu ya Anzhi Makhachkala ya nchini Urusi.

Amesema kila mmoja huko Stadio Guisseppe Meaza alifahamu Sneijder alikua katika mtego mkubwa wa kutaka kuondoka Inter Milan na kujiunga na Man utd ama Man city lakini kwa sasa wamesitishwa mpango huo.

Amesema hakuna mazungumzo yoyote yanayoendelea kwa sasa zaidi ya maandalizi ya msimu mpya wa ligi ya nchini Italia ambayo itaanza kutimua vumbi lake mwishoni mwa juma hili katika viwanja kumi tofauti.

No comments:

Post a Comment