KARIBU KWENYE BLOGU YA XTRA COVER ILI UWEZE KUFAHAMU YALE YANAYOTOKEA NJE YA MIPAKA YA NCHI YETU, PIA WAWEZA KUTOA MAONI YAKO KWA TAARIFA YOYOTE ITAKAYO KUKUNA.

Thursday, September 29, 2011

ROBERTO MARTINEZ AIKATAA MIPANGO YA KUMSAJILI DIOUF.

Meneja wa Wigan Athletics, Roberto Martinez amekanusha taarifa za kuwa mbioni kumsajili mshambuliaji kutoka nchini Senegal El-Hadji Diouf.

Roberto Martinez amekanusha taarifa hizo huku akikiri uwepo wa mshambuliaji huyo katika mazoezi ya kikosi chake ambacho kinashiriki michuano ya ligi kuu ya soka nchini Uingereza na mwishoni mwa juma hili kitashuka dimbani kucheza na Aston Villa.

Amesema El-Hadji Diouf amekua akifanya mazoezi na wachezaji wake, na hatua hiyo ilianza toka alipotemwa na klabu ya Blackburn ambayo ilichoshwa na tabia zake za utovu wa nidhamua ambazo alikua akizionyesha mara kwa mara.

Amesema mbali na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 30, pia kipa kutoka nchini Ghana Richard Kingson, amekua akifanya mazoezi na kikosi chake mara baada ya kutemwa na klabu ya Blackpool, ambayo ilishuka daraja mwishoni mwa msimu uliopita.

Hata hivyo Roberto Martinez ametoa sababu za kuwapokea wachezaji hao wawili katika mazoezi ya kikosi chake ambapo amedai kwamba uwepo wao kikosini unatoa changamoto ya uzoefu kwa wachezaji wake ambao wanahitaji msaada mkubwa katika suala hilo.

Lakini licha ya kukanusha taarifa za kutaka kumsajili El-Hadji Diouf, Roberto Martinez bado anaendelea na mchakatio wa kutaka kufanya usajili wa mchezaji mmoja ama wawili ambao watajiunga na wengine klabuni hapo kwa lengo la kuongeza nguvu ambayo inaonekana kupungua, hatua ambayo imesababisha vipigo katika michezo ya ligi.

Wakati huo huo Roberto Martinez amezungumzia mchezo wa mwishoni mwa juma hili dhidi ya Aston villa ambapo amesema utakua mchezo muhimu kwa kila upande zaidi ya masuala ya kibinafsi ya kila mtu anaehusika na mchezo huo.

Martinez amezungumzi suala hilo baada ya kuulizwa anajisikia vipi kuelekea Villa Park baada ya kuikataa ofa ya kuwa meneja wa klabu ya Aston Villa mwishoni mwa msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment